Tuesday, August 6, 2013

TATIZO LA KUPATA CHOO KIGUMU KWA WATOTO NA JINSI YA KULITATUA TATIZO HILO


NI NINI TATIZO LA KUPATA HAJA KUBWA?
Ni  haja kubwa inayopatikana isiyozidi mara tatu katika wiki na ama haja kubwa inayoleta shida kutoka kwake na utokaji wake ni mithili ya mavi ya mbuzi (uyabisi) hata kama inapatikana kila siku. Hali hii inaposhamiri muathirika hupata choo si zaidi ya mara tatu katika kipindi cha  mwezi mmoja.
Ni moja miongoni mwa matatizo katika mfumo wa kusaga chakula yanayowakumba watu wengi si hapa kwetu Zanzibar tu bali dunia nzima kwa jumla. Shida ya kupata choo ni hali inayowakabili watu mbalimbali.
SABABU
Zipo sababu kadhaa zinazopelekea kutokea kwa tatizo la kukosa kupata haja kubwa kikawaida, miongoni mwa hizo ni kama hizi zifuatazo:
  • Inaweza ikawa yenyewe tu bila kusababishwa na hali yoyote ile kama vile madhara ya dawa
fulani, au hali ya kiafya, na huwa haiambatani na maumivu ya tumbo. Kwa lugha nyengine ni kwamba sababu hasa huwa haijulikani. Hii ndio sababu maarufu kuliko nyengine zote.
  • Inaweza kusababishwa na mpangilio mbaya wa chakula, kutokula vyakula vyenye fiber (nyuzinyuzi), kunywa maji kidogo kuliko inavyotakiwa.
  • Matumizi ya dawa mbalimbali na baadhi ya athari zake kama vile baadhi ya dawa za kutibu presha (shinikizo la damu), dawa za kupunguza maumivu, dawa za kutibu degedege, dawa za kutibu mamivu ya tumbo ikiwa pamoja na dawa za kutibu mfadhaiko, dawa za kutibu alaji (makole).
  • Mgonjwa wa maradhi ya kisukari, maradhi ya misuli.
  • Maradhi ya uvimbe katika uti wa mgongo, kansa ya utumbo mkubwa, kidonda/kuchanika njia ya haja kubwa mlangoni yaani fisha (anal fissure).
  • Kwa makusudi tu mtu hujizuwia asiende haja kwa sababu labda hakuna choo cha kuridhisha, anaogopa maumivu hasa wale wenye fisha (anal fissure), ama kwa uvivu tu.
  • Watoto nao hupata tatizo la kuzaliwa nalo. Kukosekana mishipa ya fahamu katika sehemu ya utumbo mkubwa huwa ndio sababu inayopelekea utumbo huo kutosukuma kinyesi hivyo kusababisha kuchelewa kupata haja kubwa ambapo mara nyengine hupindukia kipindi cha wiki moja hadi mbili au hata zaidi. Kwa maana hiyo tumbo huvimba na mtoto hudhoofu kiafya. Hili ni tatizo la kipekee.
TIBA
Iwapo mtoto wako mchanga au mdogo ana tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu kwanza wasiliana na daktari au mpeleke hospitalini ili upate ushari wa daktari. Pia unashauriwa kujaribu njia zifuatazo:

1. Jaribu kumpa mtoto wako maji safi na salama kuanzia mililita 60 hadi 120 kwa siku. Punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa. Ni bora maji ya mtoto yachemshwe na kufunikwa vyema.
2. Iwapo maji hayasaidii, jaribu pia kumpa juisi za matunda. Mpe mtoto wako juisi ya tufaha (apple), pea au prune iliyotengenezwa kwa kutumia maji salama na safi kila siku. Anza kwa mililita 60 hadi 120 kwa siku na punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.
3. Jitahidi kumpa mwanao chakula chenye ufumwele au fiber. Iwapo mwanao ameanza kula vyakula vigumu, basi mpe vyakula vyenye ufumwele kuliko vyakula vyenye wanga, kama vile tumia unga wa shayiri au tunda la apple na pea lililopondwa pondwa vyema na kuwa kama uji. Epuka kumpa mtoto cereal ya mchele au uji wa mchele kama anatatizo la kukosa choo au kufunga choo.
4. Jiepushe kumpa mtoto wako vyakula vyenye wanga na sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa unga uliokobolewa.
5. Mpake mwanao mafuta kidogo sehemu inayotoka choo kikubwa ili kurahisisha utokaji wa kinyesi. Usitumia mafuta ya madini (mineral oil) au dawa za kulainisha choo na za kuharishwa katika kutibu tatizo hilo la kukosa choo la mtoto.
6. Kukosa choo watoto wadogo mara chache huwa kunasababishwa na magonjwa kama vile Hirschsprung ugonjwa wa kumee neva katika utumbo, au Cystic Fibrosis. Muone daktari au mpeleke mtoto wako hospitalini kama tatizo hilo la kukosa choo linaendelea hata baada ya kubadilisha aina ya chakula cha mtoto au linaambatana na dalili nyingine kama vile kutapika au mtoto kukosa utulivu na kuhangaika.
7. Kuna baadhi ya watoto wanakosa choo au kuwa na choo kigumu kutokana na kutumia maziwa ya ng’ombe. Iwapo umetumia dawa na umefuata maelekezo ya kuondoa ukosefu wa choo na hukufanikiwa. Katisha kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe kwa siku mbili au tatu, baada ya siku hizo iwapo bado hajaacha choo badi endelea kumpa maziwa hayo, na pengine tatizo hilo halisababishwi na maziwa ya ng’ombe.
8. Mwogeshe au mweke mwanao katika beseni la maji ya uvuguvugu na hakikisha maji yanafika hadi kifuani. Mkande mtoto tumbo lake wakati akiwa majini na njia hiyo husaidia kulegeza misuli ya mwili wa mtoto, na kumsaidia kupata chook wa urahisi.
N.B Ukosefu wa choo kwa watu wazima baadhi ya wakati huandamana na magonjwa kama vile Arthritis, Appendicitis, Cataract, saratani, shinikizo la damu, Rheumatism na kadhalika lakini kwa watoto huenda tatizo hilo likawa halisababishwi na maradhi hayo.
Utafiti unaonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kuhusu kukosa choo mtoto na kupewa nyongeza ya chuma au Iron Supplement. Hivyo usimkatishe kumpa mwanao chuma iwapo anakosa choo. Kwani chum ni muhimu sana katika kuzuia upungufu wa damu mwilini kwa mtoto wako mdogo.

No comments:

Post a Comment